Benki ya TADB yatoa mkopo kwa wafugaji wa Mji wa Korogwe
Chama cha Ushirika cha Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Mjini Korogwe (UWAKO) kimepata mkopo wa ng’ombe thelathini wa maziwa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB). Mkopo huo wa ng’ombe thelathini una thamani ya Shilingi Milioni Sitini na mkopo utalipwa kwa muda wa Miaka Mitatu. Wanachama waliokithi vigezo wamekabidhiwa ng’ombe hao Februari 5, mwaka huu katika ofisi za chama cha UWAKO ziliyopo eneo la Majengo.
“Vijana tunatakiwa kuchangamkia fursa za ufugaji ili kujikomboa kiuchumi” alisema Bi. Farida Ponda ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha ushirika cha ufugaji wa ng'ombe wa maziwa Mji wa Korogwe (UWAKO). Bi. Farida alifafanua kuwa Lengo kuu la Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) kutoa mkopo wa go’ombe wa maziwa kwa wafugaji hao ni kuimarisha kipato cha wafugaji na sekta ya mifugo kwa ujumla hapa nchini katika harakati za kuelekea uchumi wa viwanda.
“ Wafugaji mjiepushe kuwatumia madaktari vishoka (madakatari wa mtaani) kutibu ng’ombe zenu” alisema Dr. Fortunatas Silayo ambaye ni Afisa Mifugo kutoka Halmadhauri ya Mji wa Korogwe wakati akikabidhi ng’ombe hao kwa wanachama wa UWAKO. Dr. Silayo alisisitiza zaidi kwa kusema “ili mfugaji upate maziwa ya kutosha ni vyema kuwapa ngombe malisho bora pamoja na kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa mifugo”.
Kwa upande mwingine Ndugu Denisi Nguruse ambaye ni Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alitoa nasaha kwa wanufaika wa mkopo wa ng’ombe kwa kusema “mhakikishe ng’ombe mliopewa mnawaweka kwenye mabanda bora”. Nae Bi. Yusta Luoga ambaye ni mnufaika wa mkopo wa ng’ombe wa maziwa aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Ushirika wa UWAKO kwa ujumla kwa kufungua fursa za kiuchumi kwa vijana wa Mji wa Korogwe.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.