Mkuu wa wilaya ya Korogwe Bi. Kissa Kasongwa amewataka madiwani wa Halmashauri ya mji wa Korogwe kuendelea kushirikiana na watumishi kuanzia ngazi ya serekali za mitaa hadi mkurugenzi ili waweze kutatua changamoto za wananchi kama vile elimu, afya , maji na miundombinu.
Akizungumza katika kikao cha madiwani cha robo ya pili ya mwaka kilichofanyika jana katika ukumbi wa halmashauri ya mji wa Korogwe alisema “madiwani wanapaswa kufanya kazi na watumishi waliopo katika kata zao kwa pamoja” akitoa mfano wa ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo ambapo alianisha kuwa halmashauri ya mji iliweza kumaliza vitambulisho 1500 walivyopangiwa na Mkoa na kuwataka waendelee kushirikiana kugawa vingine walivyopewa tena.Pia aliagiza ujenzi wa kituo cha afya cha majengo, vyumba vya madarasa na miundombinu mingine ya shule za sekondari na msingi vikamilike muda uliokusudiwa ili changamoto za afya na elimu zipungue.
Naye katibu tawala wa Wilaya ya Korogwe Bi.Rehema Mbwasi alisema kuwa taratibu za kukabidhiana hospitali ya Magunga ambayo kwa sasa inaendeshwa na halmashauri ya Wilaya ya Korogwe vijijini zimekamilika ila anasubiriwa Mhe. Mbunge ambaye yupo kwenye vikao vya bunge ili wafanye mkutano wa pamoja kati ya halmashauri ya mji na vijijini.Pia alisema mchakato wa maombi ya wanakijiji wa Kwemasimba kutaka kujumuishwa katika eneo la halmashauri ya mji badala ya halmashauri ya Korogwe vijijini umeshafikia pazuri baada ya kamati iliyoundwa kwa ajili ya suala hilo kuwazilisha taarifa yake.
Aidha mwenyekiti wa halmashauri Mhe. Hilary Ngonyani kabla ya kuruhusu maamuzi na mapendekezo ya kamati mbalimbali za madiwani kuwasilishwa; alisema kuwa tayari alishaongea na Mkurugenzi wa maji Tanga na kumhakikishia kwamba kuhusu suala la usambazaji wa maji katika mji wa Korogwe tayari lipo katika hatua ya zabuni.Pia akipokea taarifa ya mapato na matumizi kutoka kamati ya fedha na utawala ilionekana kuwa Halmashauri imekusanya kiasi cha Tsh 78,942,456 kutoka mapato ya ndani na imepokea ruzuku ya Tsh 1,306,396,350 toka serekali kuu na kufanya jumja ya mapato kwa mwezi Decemba, 2018 kuwa 1,385,339,106 na hivyo mapato kuanzia july 2018 hadi Decemba 2018 kuwa 8,560,103,545.65 sawa na asilimia 35.28 ya makisio ya Tsh 24,261,132,948.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.