Hospitali ya KCMC yatoa matibabu ya macho Mji wa Korogwe
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC iliyopo Moshi Mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Korogwe imetoa matibabu ya macho kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe na Maeneo ya jirani. Matibabu hayo ya Macho yalijumuisha uchunguzi wa macho kwa ujumla, upasuaji wa mtoto wa jicho, utoaji wa miwani pamoja na utoaji wa dawa za macho. Matibabu yalitolewa kuanzia Juni 14 na yataendelea hadi Juni 17 mwaka huu katika Kituo cha Afya cha Majengo kilichopo Kata ya Majengo.
“Hospitali ya Rufaa ya KCMC tumejipanga vyema kuhakikisha tunatatua matatizo ya macho kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe na Kanda ya Kaskazini kwa ujumla” alisema Dr. Alex Lissu ambaye ni Mratibu wa Huduma za Macho ya Kliniki Tembezi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC. Dr Lissu alitoa nasaha kwa kusema “mtoto wa jicho na matatizo ya macho kwa ujumla yanatibika hivyo wanachi wa Mji wa Korogwe wajitokeze kwa wingi ili tuwapatie matibabu”.
Kwa upande mwengine, Dr. Alex Lissu alifafanua kuwa kwa siku Nne mfululizo waliopo Kituo cha Afya cha Majengo walipanga kuwafanyia uchunguzi wa macho watu Mia Nne na kuwafanyia upasuaji wa macho watu Mia Moja. Pia alifafanua zaidi kuwa Wananchi wengi waliofanyiwa uchunguzi wa macho walibainika kuwa na matatizo ya macho ikiwa ni pamoja na mtoto wa jicho, matatizo ya macho kwa watu wazima, na presha ya macho. Matatizo mengine ni ukungu wa macho, upungufu wa kuona, pamoja na shida ya macho inayosababiswa na sukari.
“Tunatoa shukrani kwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa kuwapatia matibabu ya macho Wananchi wa Mji wa Korogwe” alisema Dr. Theresia Mauya ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Majengo. Dr. Mauya alifafanua kuwa ushirikiano kati ya Hospitali ya Rufaa ya KCMC na Halmashauri ya Mji wa Korogwe katika matibabu ya macho ni wa kindugu na utakuwa ni endelevu katika kutatua changamoto ya macho kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe.
Nae Ndugu. Lucas Zimamoto ambaye ni Mratibu wa Matibabu ya Macho katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “ muitikio wa Wananchi waliojitokeza kupatiwa matibabu ya macho kwa gharama nafuu ni mzuri”. Kwa upande mwengine, Mzee Fadhili Chiliavyangu ambaye ni Mwananchi wa Mji wa Korogwe aliyejitokeza kupatiwa matibabu alisema “tunatoa shukrani kwa Wataalamu wote kutoka Hospitali ya Rufaa ya KCMC pamoja na Wataalamu wa Kituo cha Afya cha Majengo kwa kutupatia matibabu ya macho kwa gharama nafuu”.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.