Komba: Madiwani pamoja na Wataalamu twendeni kwa Wananchi tukahamasishe Sensa
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Mhe. Francis Komba amewataka Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kuunga mkono jitihada za Serikali katika ushiriki pamoja uhamasishaji wa zoezi la Sensa linalotatarajiwa kufanyika Agosti 23, Mwaka huu. Agizo hilo alilitoa wakati wa Baraza la Madiwani la Kawaida la Robo ya Nne linalohitimisha Mwaka wa Fedha 2021/22 lililofanyika Julai 28, Mwaka huu katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
“Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri twendeni kwa Wananchi tukahamasishe Sensa” alisema Mhe. Francis Komba ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Diwani wa Kata ya Mtonga wakati wa Baraza la Madiwani. Mhe. Komba alifafanua kuwa zoezi la Sensa ni jambo la kimaendeleo hivyo Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri wanatakiwa kushiriki pamoja kuhamasisha Wananchi waweze kuhesabiwa ili Serikali iweze kufanikisha malengo iliyojiwekea katika kuwahudumia Wananchi wake.
“Mheshimiwa Mwenyekiti maagizo yote uliyotupa tumeyapokea na tutayafanyia kazi” alisema Ndugu Frank Fuko ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Ndugu Fuko alifafanua kuwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe imejipanga vyema katika kuhakikisha inatekeleza kikamilifu zoezi la Sensa linalotajajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu ili kupata takwimu halisi za Watu na Makazi kwa maendeleo ya Mji wa Korogwe na Nchi kwa ujumla.
Kwa upande mwengine, Mhe Mustafa Shengwatu ambaye ni Diwani wa Kata ya Majengo alisema “Madiwani wa Mji wa Korogwe tayari tumeshaanza na tunaendelea na zoezi la uhamasishaji wa Sensa kwa Wananchi”. Mhe. Shengwatu alisisitiza kuwa Madiwani wote kwa sasa wamejiwekea mkakati kila wanapokuwa na kikao chochote iwe ni ngazi ya Kata au kinachohusisha Wananchi moja kwa moja ushiriki wa Sensa ni agenda mojawapo itakayozungumzwa katika kikao hicho.
“Natoa pongezi kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kwa kuwahimiza Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri kuongeza nguvu katika uhamasishaji wa Sensa” alisema Bw. Maurice Frank ambaye ni Mwananchi wa Mji wa Korogwe aliyeshiriki katika Baraza la Madiwani la Robo ya Nne linalohitimisha mwaka mwa fedha 2021/22. Bw. Maurice alifafanua kuwa iwapo kila Diwani katika eneo lake na kila Mtaalamu wa Halmashauri kwa nafasi yake atafanya jitihada za uhamashishaji wa zoezi la Sensa kwa Wananchi, Wananchi watahamasika na watashiriki ipasavyo katika kuhesabiwa.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.