Madiwani, Mkurugenzi wa Mji wa Korogwe watembelea miradi ya maendeleo
Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wakiambatana na Mkurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara mbalimbali wametembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni ziara yao ya kwanza baada ya kuingia madarakani katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025. Lengo kuu la ziara hiyo ni kuangalia namna miradi hiyo ilivyokamilika na mafanikio yake kwa wananchi. Ziara hiyo imefanyika Januari 19, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Korogwe.
“Kwa kiasi kikubwa miradi hii ya elimu imesaidia kupunguza baadhi ya changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi” alisema Mhe. Fancis Komba ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Diwani wa Kata ya Mtonga wakati akikagua miradi ya ujenzi wa Madarasa, mabweni pamoja na matundu ya vyoo. Mhe. Komba alitoa msisitizo kwa walimu kwa kusema “walimu fanyeni kazi kwa bidii na hakikisheni ufaulu wa wanafunzi unaongezeka katika shule zenu”.
Katika ziara hiyo, miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Kimweri, ujenzi madarasa pamoja na mabweni katika Shule ya Sekondari Semkiwa pamoja na ujenzi wa shule ya Sekondari Bagamoyo. Miradi mingine ni ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule za Msingi Matondoro, Mgombezi pamoja na Bagamoyo.
Miradi mingine ni pamoja na mradi wa ufugaji wa nyuki katika eneo la Kwameta unamilikiwa na kikundi cha Silabu Beekiping kilichopo Kata ya Old Korogwe, mradi wa uchimbaji wa kisima cha kutikisa katika Mtaa wa Mbeza, mradi wa Kituo kikubwa cha mabasi Kilole, mradi wa Soko la Kilole pamoja na mradi wa vyoo vya umma katika Soko la Manundu.
“Kadri fedha zitakavyopatikana tutawekeza katika miradi mbalimbali ili kupunguza baadhi ya changamoto kwa wananchi” alisema Bi. Bernadetha January ambaye ni Mchumi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na anaemuakilisha Mkurugenzi wakati wa ziara hiyo. Bi. January alifafanua zaidi kwa kusema “baadhi ya miradi sio tu itasaidi wananchi kupata huduma lakini pia itasaidia kuongeza mapato katika Halmashauri”.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.