Madiwani, Mkurugenzi wa Mji wa Korogwe watembelea miradi ya maendeleo
Madiwani, Mkurugenzi pamoja na Wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wametembelea miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ziara za kutembelea miradi katika kipindi cha Robo ya Kwanza kwa Mwaka wa fedha 2021/2022. Ziara hiyo ya kutembelea miradi imefanyika Oktoba 26, Mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Korogwe.
Katika ziara hiyo miradi iliyotembelewa ilijumuisha Mradi wa Ujenzi wa Uzio wa matofali ya saruji katika Kituo cha Afya cha Majengo wenye thamani ya Shilingi Milioni 21, Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi wenye thamani ya Shilingi Milioni 500, ambapo Serikali tayari imeshatoa Shilingi Milioni 250 za awali kwaajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Madiwani, Mkurugenzi pamoja na Walaalamu pia walitembelea Mradi wa Kiwanda cha kutengeneza tofali za saruji kinachomilikiwa na Halmashauri ya Mji wa Korogwe wenye thamani ya Shilingi Milioni 93 uliopo eneo la Bagamoyo jirani ya Kituo cha Mabasi cha Balozi John Kijazi. Kiwanda hicho cha tofali kinauwezo wa kuzalisha tofali Elfu Nne kwa siku moja.
“Natoa pongezi kwa kamati yote inaayosimamia mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi, mradi unaendelea vyema” alisema Mhe. Francis Komba ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Diwani wa Kata ya Mtonga wakati wa ukaguzi wa miradi. Mhe. Komba alifafanua kuwa mradi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi utakapokamilika utakuwa mkombozi kwa Wananchi wa Kata ya Mgombezi na maeneo ya jirani katika kuwapatia huduma za afya kwa ukaribu zaidi.
“Wananchi waunge mkono jitihada za serikali katika ujenzi wa miradi kwa kuchangia nguvu kazi” alisema Bi. Bernadetha January ambaye ni Mchumi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe aliyemuwakilisha Mkurugezi wakati wa ziara ya kutembelea miradi. Bi. January alisisitiza kuwa iwapo Wananchi watashiriki ipasavyo katika kuchangia nguvu kazi wakati wa utekelezaji wa miradi, watasaidia miradi kukamilika kwa wakati na kupunguza gharama za fedha.
Katika hatua nyengine, Bi.Khadija Runza ambaye ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Majengo aliishukuru Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Serikali kwa ujumla kwa kutekeleza mradi wa Ujenzi wa uzio katika Kituo cha Afya cha Majengo. Bi.Khadija alifafanua kuwa ujenzi wa uzio huo utasaidia kuimarisha ulinzi katika kituo hicho.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.