Mji wa Korogwe wagawa vitatambulisho vya wajasiriamali
Halmashauri ya Mji wa Korogwe imeanza mchakato wa kugawa vitambulisho vipya vya wajasiriamali kwa wafanya biashara wadogo wa Mji wa Korogwe. Mchakato wa ugawaji wa vitambulisho kwa Watendaji wa Kata zote kumi na moja (11) ambao ndio watawakabidhi wajasiriamali ulifanyika Mei 28, mwaka huu katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Akizungumzia mchakato huo wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo Ndugu Rahel Muhando ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya alisema “ wafanyabiashara wadogo ni vyema wakapatiwa vitambulisho kwa wakati ili wawe huru katika kufanya biashara zao bila ya usumbufu wowote”. Vilevile alitoa ushauri kwa watendaji wa Kata kutunza takwimu za wajasiriamali katika maeneo yao ili kuwatambua wajasiriamali wao.
Nae Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “Halmashauri ya Mji wa Korogwe tumepokea vitambulisho 513 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga na vitambulisho hivi vitagaiwa kwa wajasiriamali kupitia watendaji wa Kata waliopo kwenye maeneo yao”. Kwa upande wa watendaji wa Kata waliahidi kufanya kazi kwa ufanisi kuhakikisha serikali inafikia malengo yake katika mchakato wa ugawaji wa vitambulisho vya wajasiriamali.
Vitambulisho vya kipindi hiki vitakuwa vinatolewa kwa njia ya mtandao ambapo malipo yote yatafanyika kupitia Benki, Wakala wa Benki au Simu Pesa.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.