Mji wa Korogwe wapata mafunzo ya TASAF kunusuru kaya masikini
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji wa Korogwe wametoa mafunzo kwa viongozi na watendaji mbalimbali watakaoshiriki katika mchakato wa kunusuru kaya masikini katika Halmashauri ya mji wa Korogwe. Mafunzo hayo ya siku mbili yalitolewa kuanzia Juni 16 hadi 17, mwaka huu katika ukumbi wa Halmashaauri ya Mji wa Korogwe.
Lengo la mafunzo hayo ya siku mbili ni kujenga uelewa kwa viongozi na watendaji mbalimbali watakaoshiriki katika mchakato wa Tasaf kuanzia ngazi ya Kata, Mitaa hadi Vijiji ili kufanya kazi kwa ufanisi. Mpango huu wa Tasaf ni muendelezo wa mikakati yake ya kupunguza umasikini katika jamii ambapo kwa mwaka huu ni kipindi cha pili cha awamu ya tatu kinachotekelezwa kwa miaka minne kuanzia mwaka 2020 hadi 2023.
Akizungumzia mafunzo hayo Ndugu Rahel Muhando anayemuakilisha Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mh. Kissa Kasongwa alisema “viongozi pamoja na watendaji wote tunaoshiriki katika mchakato wa Tasaf lazima tukatende haki, tuwe wazalendo pamoja na kufanya kazi kwa uadilifu” Kwa upande mwingine, Ndugu Frank Fuko anayemuakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “nina Imani kubwa mafunzo yaliyotolewa yameeleweka vizuri, ni vyema washiriki mkafanye kazi kwa ufanisi"
Nae ndugu Victor Manyai ambaye ni muezeshaji wa mafuzo hayo alitoa ushauri kwa washiriki kwa kusema "watendaji wa Tasaf ni vyema kujiepusha na udanganyifu wowote na yeyote atakayebaika sheria itachukua mkondo wake. Nao washiriki walitoa shukrani kwa kupatiwa elimu ya namna ya kushiriki katika mpango wa kunusuru kaya masikini na kuahidi kufanya kazi kwa umakini.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.