Mji wa Korogwe watangaza fursa za uwekezaji
Halmashauri ya Mji wa Korogwe imetangaza fursa za uwekezaji katika hatua za kukuza uchumi wa kati na kuunga mkono jitihada za Mh. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda hapa nchini. Fursa hizi za uwekezaji zilitangazwa Oktoba 22, mwaka huu wakati wa mkutano wa Baraza la biashara la wilaya ya Korogwe katika ukumbi wa hoteli ya Korogwe Executive Lounge uliopo eneo la Kwamkole.
Akizungumzia fursa hizi ndugu Ramadhani Sekija afisa kilimo wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kwa niaba ya Mkurugenzi alisema milango iko wazi kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika Mji wa Korogwe ambapo wameandaa mazingira mazuri na yenye tija kwa wawekezaji. Ndugu Sekija alianisha maeneo ya uwekezaji kama vile kilimo cha umwagiliaji, kilimo cha matunda na mbogamboga, ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, ufugaji wa nyuki, viwanda, ujenzi wa hoteli za kitalii pamoja na elimu.
Nae ndugu Farijala Msangi ambaye ni afisa biashara wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema kuna fursa nyingi za kiuchumi ambapo wawekezaji mbalimbali wanaweza kuzichangamkia. Ndugu Msangi alisema kuna eneo kubwa la kilimo cha umwagiliaji, ambapo hekta 520 eneo la mahenge , hekta 210 eneo la Kwamngumi na hekta 420 eneo la Lwengera. Pia alizungumzia kilimo cha matunda na mbogamboga na kusema kuwa kuna ardhi ya kutosha katika maeneo ya Ngombezi, Mtonga, Old Korogwe pamoja na Kwamsisi.
Katika Sekta za viwanda, ndugu Msangi alisema katika Mji wa Korogwe yapo maeneo ya kutosha kwa ajili ya viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ambapo kuna mita za mraba 9000 eneo la Old Korogwe na hekta 2000 eneo la Ngombezi. Hata hivyo aliwatoa hofu wawekezaji kuhusu malighafi na kusema kuna malighafi za kutosha kutoka wilaya za jirani vilevile Mji wa Korogwe ni lango kuu la kupitisha bidhaa mbalimbali kutoka mikoa ya kaskazini hivyo kuwa na uhakika na malighafi za kutosha.
Akizungumzia fursa za Elimu ndugu Msangi alisema kuwa Mji wa Korogwe unakua kwa kasi na kuna uhitaji mkubwa wa taasisi za elimu kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu. Katika eneo la Old Korogwe kumetengwa eneo la ekari 45 kwa ajili ya shule na vyuo vya kati na ekari 77 kwajili ya vyuo vikuu. Kwa upande mwingine Mh. Hillary Ngonyani ambaye ni mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alitoa wito kwa wenyeji wa Korogwe na watanzania wote kuchangamkia fursa ya viwanja kwa ajili ya makazi na biashara vilivyopo eneo la Bagamoyo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.