Mji wa Korogwe watoa Mkopo wenye thamani ya Shilingi Milioni 97
Halmaashauri ya Mji wa Korogwe katika Mwaka wa Fedha 2022/ 23 imetoa mkopo wenye thamani ya Shilingi Milioni Tisini na Saba kwa Vikundi Kumi na Sita vya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu. Mkopo huo ni sehemu ya Asilimia Kumi ya Mapato ya ndani na ikiwa pia ni agizo la Kisheri. Mgeni rasmi katika utoaji wa Mkopo huo alikua Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mhe. Dkt Alfred Kimea. Halfa ya utoaji Mkopo huo imefanyika Januari 11, Mwaka huu katika Uwanja vya Sokoni uliopo Kata ya Manundu.
Vikundi vilivyonufaika na Mkopo wa kiasi cha Shilingi Milioni Tisini na Saba kutoka Halmashauri vinajihusisha na shughuli mbalimbali za Kiuchumi ikijumuisha Uuzaji wa nafaka , Usafirishaji wa abiria na mizigo, pamoja na Kilimo cha matunda na mbogamboga. Shughuli nyingine ni Ufugaji wa kuku, Ubunifu wa Mavazi ( ushonaji wa nguo) pamoja na Kazi mbalimbali za ufundi.
“Serikali imedhamiria kwa dhati kuwawezesha Kiuchumi Watu wa Hali ya chini ikijumuisha pia na Watu wenye ulemavu” alisema Mhe. Dkt. Alfred Kimea ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini wakati akikabidhi Hundi ya Shilingi Milioni Tisini na Saba kwa wahufaika wa Mkopo huo. Mhe. Dkt. Kimea alisisitiza kuwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu wachangamkie fursa ya Mikopo ya Halmashauri ambayo ina masharti nafuu kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
“ Halmashauri imefanya jitihada za utoaji wa Mkopo wa Asilimia Kumi kwa kuzingatia usawa ikihusisha Vikundi kutoka Kata zote za Mji wa Korogwe” alisema Bw. Frank Fuko ambaye ni Kaimu Mukurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Bw. Fuko alifafanua kuwa Halmashauri itaendelea na jitihada za utoaji wa Mikopo kadri fedha zitakapopatikana.
Kwa upande mwengine, Bi. Rehema Letara ambaye ni Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alitoa nasaha kwa wanufaika wa Mikopo kwa kusema “ Wanufaika wote wa Mikopo hakikisheni mnarejesha mikopo kwa wakati ili Wananchi wengine waweze kunufaika na mikopo hiyo” Nae Bw. Mwanga Ntandu ambaye ni mnufaika wa Mikopo mwenye uoni haifu alitoa shukrani kwa kusema “Watu wenye ulemavu tunatoa shukrani kwa Halmashauri na Serikali kwa ujumla kwa kutupatiwa mikopo yenye masharti nafuu, mikopo hii itatusaidia kujikwamua kiuchumi” .
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.