Mji wa Korogwe waungana na Mataifa mengine kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani
Mji wa Korogwe leo umeungana na Mataifa mbalimbali Ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani. Siku hii huadhimishwa kila Mwaka ifikapo Tarehe Moja ya Mwezi Desemba . Lengo la maadhimisho hayo ni kutoa elimu kuhusu namna ya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, kupiga vita unyanyapaa pamoja na kuhimiza Watu kwenda kufanya vipimo ili kufahamu afya zao. Katika Mji wa Korogwe maadhimisho hayo yamefanyika katika Soko la Msambiazi lililopo Kata ya Mtonga. Kauli mbiu ya Mwaka huu ni “Imarisha Usawa”.
“Nitoe rai kwa Vijana na Watu wote kwa ujumla kujikinga na janga hili la Ukimwi” alisema Mhe. Andrew Gao ambaye ni Diwani wa Kata ya Masuguru aliekuwa Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Mwaka huu. Mhe Gao alisisitiza kuwa ni vyema kila mmoja akawa na tahadhari na afya yake, tahadhari hiyo itamfanya Mtu kuwa makini sio tu kujikinga na ugonjwa wa Ukimwi bali pia na magojwa mengine.
Nae Bi. Charity Sichona ambaye ni Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe aliyemuakilisha Mkurugenzi katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani alisema “ tujiupushe na tabia ya kunyoosheana vidole katika Jamii, kumnyoshea kidole Mtu kwa dhana ya kuwa ni mwathirika wa Ukimwi ni unyanyapaa na pia ni ukatili mkubwa wa kijinsia”. Bi. Charity alisisitiza kuwa ni vyema Watu wenye ugonjwa wa Ukimwi tukaishi nao kwa furaha na upendo kama walivyo Watu wenye maradhi mengine.
“Ni vyema tukapima afya zetu kabla ya kufunga ndoa” alisema Bw. Lawi Mshana ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Victorius Life Ministries akiyeshiriki katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani mwaka huu. Bw. Mshana alifafanua kuwa kunafuraha kubwa iwapo Mtu ataingia kwenye ndoa huku akiwa anafahamu afya yake. Nae Bi. Saumu Kingu ambaye ni Mwananchi wa Mji wa Korogwe aliyeshiriki katika Maadhimisho hayo alitoa shukrani kwa Serikali na Asasi zote za Kiraia kwa kufanikisha vyema Maadhimisho ya Mwaka huu.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.