Viongozi wa Dini, Watendaji waunga mkono utoaji wa chanjo ya Uviko -19
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya Dini katika Mji wa Korogwe, Wahamasishaji wa maswala ya kijamii, Vyombo vya Habari pamoja na Watendaji wa Kata, Mitaa, na Vijiji wameiunga mkono Serikali katika Kampeni ya utoaji wa chanjo ya Uviko -19 nyumba kwa nyumba ili kuwapatia chanjo wananchi kwa urahisi zaidi. Uungaji mkono huo waliutoa wakati wa Kikao Kazi cha maswala utoaji wa Chanjo ya Uviko -19 kilichofanyika Septemba 28, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Kikao Kazi hicho cha maswala ya utoaji Chanjo ya Uviko -19 kiliitishwa na Serikali kwa lengo la kutoa mafunzo ya mpango harakishi na shirikishi wa Chanjo ya Uviko -19 kwa wadau mbalimbali ili kuiunga mkono Serikali katika Kampeni ya utoaji wa Chanjo nyumba kwa nyumba itakayodumu kwa Siku Kumi na Nne, ambapo utaratibu tayari ulishaanza tokea Septemba 22, na utamalizika Oktoba 05, mwaka huu. Baada ya Kampeni kumalizika huduma zitaendelea kutolewa kama kawaida katika Vituo vyote vya kutolea Chanjo vilivyoainishwa.
“Nyie ndio mnaoishi na wananchi kwa ukaribu zaidi, nendeni mkatusaide kuwaelimisha ili tuwapatie chanjo” alisema Dkt. Salma Sued ambaye ni Mganga Mkuu wa Halamshauri ya Mji wa Korogwe. Dkt. Sued alifafanua kuwa Chanjo ya Uviko -19 ni salama kwa matumizi ya binadamu na haina madhara yoyote hivyo Wananchi wasiwe na hofu yoyote.
“Natoa pongezi kwa waandaaji wa kikao, wametuelimisha na kutuhamasisha vyema na sisi tutakwenda kuwaelimisha Wananchi ili wajitokeze kwa wingi kupatiwa Chanjo ya Uviko -19” alisema Mzee Mohamed Dodoa ambaye ni Mhamasishaji Maarufu wa maswala ya kijamii katika Mji wa Korogwe. Mzee Dodoa alifafanua kuwa Serikali imefanya jambo jema kuwashirikisha Viongozi wa Dini, Wahamasishaji, Vyombo ya Habari pamoja na Watendaji wa Kata, Mitaa na Vijiji kwani wao ndio wanaoishi na wananchi kwa ukaribu zaidi.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.