Wananchi wa Mji wa Korogwe wakabidhiwa hati zao za viwanja
Halmashauri ya Mji wa Korogwe kupitia Idara ya Ardhi na Mipango Miji imekabidhi hati za viwanja takribani 107 kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe. Hati hizo za viwanja zimetolewa Septemba 24, mwaka huu katika Ofisi za Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Akizungumzia mchakato huo wa hati Bi. Joanitha Kazinja ambaye ni Msajili Msaidizi wa Hati Mkoa wa Tanga alisema "kila mwananchi mwenye eneo ambalo limepimwa na idara ya ardhi na mipango miji na kufata taratibu zote atapatiwa hati yake ya umiliki wa ardhi". Bi.Kazinja alitoa ushauri kwa wananchi kwa kusema "wananchi mnapotaka kununua viwanja ni vyema kufika ofisi za ardhi na mipango miji kwa lengo la kuhakiki eneo husika ili kujiepusha na matapeli".
Nae Ndugu Nyambega Kichele ambaye Afisa Ardhi Mteule Katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema "mchakato wa ugawaji wa hati za viwanja unakwenda sambamba na zoezi linaloendelea la urasimishaji wa makazi katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Korogwe". Ndugu Kichele alifafanua kuwa hati za ardhi zilizotelewa zinahusisha viwanja vya maeneo ya Mtonga Chini, Mtonga Semkiwa, Bagamoyo Viwanja vipya pamoja na Kilole Manzese.
Kwa upande mwingine, Wananchi mbalimbali wa Mji wa Korogwe ambao wamekabidhiwa hati zao za viwanja waliwashukuru Maafisa wa Ardhi na Mipango Miji pamoja na Serikali kwa ujumla kwa kuwamilikisha maeneo yao kihalali.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.