Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa waapishwa
Wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe wameapishwa ili kuanza rasmi zoezi la kuandikisha wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.
Kiapo hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa kimefanyika Septemba 23 katika ukumbi wa mikitano wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Katika kiapo hiki, wasimamizi wasaidizi waliapa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe Ndugu. Musa Jonathan Ngalu ili kufanya kazi kwa kufuata kanuni na sheria za uchaguzi.
Kwa upande mwingine msimamizi wa uchaguzi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe Bwana Kasimu Kaoneka amewasihi wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kufanya kazi kwa weledi huku wakifuata kanuni na sheria za uchaguzi. Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi wa serikali za mitaa zoezi la kuandikisha wapiga kura linatarajiwa kuanza Oktoba 8, na kumalizika Oktoba 14 mwaka huu. Vituo vitakavyotumika kuandikisha wapiga kura baadae vitatumika kuwa vituo vya kupigia kura. Vilevile wakati wa kuandikisha vituo vitafunguliwa saa mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni.
Nae Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Bwana Charles Mtali amewasisitiza wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwa makini na ratiba ya kuendesha mikutano ya kampeni za uchaguzi. Bwana Mtali alisema kipindi cha kufanya mikutano ya kampeni kitakuwa ni muda wa siku saba kabla ya siku ya uchaguzi ambapo itakuwa ni Novemba 17 hadi 23 mwaka huu.
Bwana Mtali aliendelea kufafanua kuwa kila chama cha siasa kitakachishiriki uchaguzi kitatakiwa kuwasilisha ratiba yake ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi kwa msimamizi wa uchaguzi si chini ya siku saba kabla ya kuanza kwa kampeni.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.