Madiwani, Wataalamu wa Halmashauri watakiwa kusimamia miradi kwa ufanisi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Mhe. Francis Komba amewataka Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanishi ili iweze kuleta jita iliyokusudiwa na Serikali. Maelekezo hayo aliyatoa wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika Novemba 03, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Kikao hicho cha Baraza la Madiwani kilikaliwa kwa lengo la kuhitimisha Robo ya Kwanza kwa Mwaka wa fedha 2021/22.
“Madiwani, pamoja na Wataalamu wa Halmashauri simamieni miradi ya maendeleo kwa ufanisi ili iweze kuleta tija kwa Wananchi” alisema Mhe. Frascis Komba ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Diwani wa Kata ya Mtonga wakati wa Kikao cha Baraza la Madiwani. Mhe. Komba alifafanua kuwa endapo miradi ya maendeleo kama vile miradi ya elimu na afya ikisimamiwa kwa ufanisi, miradi hiyo inaweza kujengwa kwa kiwango na kumalizika kwa wakati.
Katika hatua nyingine Mhe. Francis Komba alisisitiza kuwa Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo, fedha hiyo inapaswa kwenda katika eneo husika ili Serikali iweze kutimiza lengo lake. Iwapo Madiwani au Wataalamu wa Halmashauri wakienda kinyume na maelekezo ya mradi husika Serikali itachukua hatua kali za kisheria. Mhe Komba alisema “wenzetu wa TAKUKURU mmewasikia wakitupatia elimu ya usimamizi wa miradi ya maendeleo, natumaini kila mmoja wetu elimu ile ataifanyia kazi”
“Sisi kama Halmashauri tumejipanga vyema katika usimamizi wa miradi ya maendeleo” alisema Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Ndugu Bei alifafanua kuwa licha ya kupokea fedha zinazotolewa na Serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Halmashauri pia imeanzisha mradi wa utengenezaji wa matofali kwa fedha za ndani kwa lengo la kuongeza vyanzo vya mapato katika Halmashauri hiyo.
Nae Ndugu Fulgence Komba ambaye ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mhe. Dkt. Alfred Kimea aliishukuru Serikali kwa kuipatia fedha Halmashauri ya Mji wa Korogwe kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo. Ndugu Komba alisisitiza kuwa jukumu la usimamizi wa miradi ya maendeleo haliwahusu Madiwani na Watalaamu wa Halmashauri pekeyao, Wananchi pia wanatakiwa kushiriki ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.