Mji wa Korogwe wapata Mradi wa ujenzi wa mfumo wa kisasa wa Maji Taka
Shirika la BORDA linatarajia kutoa fedha kiasi cha Shilingi Milioni 246 kwa ajili ya Ujenzi wa Mradi wa Mfumo wa Kupokea, Kuchakata na Kutibu Maji Taka katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Utekelezaji wa Ujenzi wa Mradi huo ulitangazwa Januari 10, Mwaka huu wakati Kamati ya Mipango Miji na Mazingira wakiwa na Uongozi wa Shirika la Maji Safi na Usafi wa Mazingira Korogwe (KUWASA) ambao ndio wasimamizi wa Ujenzi pamoja na Uendeshaji wa Mradi huo walipotembelea Kata ya Bagamoyo kwa ajili ya ukaguzi wa eneo la mradi.
“Mradi huu utakapokamilika licha ya kutunza mazingira pia utasaidia kutoa ajira kwa Wananchi ” alisema Bw. Michael Ntulo ambaye ni Mhandisi kutoka Shirika la KUWASA ambao ndio wenye dhamana ya usimamizi wa mradi huo. Bw. Ntulo alifafanua kuwa Ujenzi wa Mradi huo utaambatana na upatikanaji wa Gari pamoja na Guta la kubebea Maji Taka ambapo Gari na Guta hilo litatumika kubeba Maji Taka kutoka kwa Wananchi kwa gharama nafuu ili kupunguza gharama za uchukuzi ukilinganisha na ghrama zinazotumika kwa sasa.
Akizungumzia utekelezji Mradi wa Ujenzi Mfumo wa Kisasa wa Maji Taka Katika Mji wa Korogwe Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe Bi. Rahel Muhando alisema “ Ujenzi wa Mfumo wa Kisasa wa Maji Taka katika Mji wa Korogwe ni jambo jema na Mradi huu utakuwa na tija kwa Wananchi. Mimi natoa baraka zote kwa ajili ua utekelezi wa Mradi huu”.
“Madiwani pamoja na Wataalamu wote wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe tunatoa shukrani kwa Shirika la BORDA kwa kutupatia Mradi wa Ujenzi wa Mfumo wa Kisasa wa Maji Taka, Mradi tumeupokea na tuko tayari kwa utekelezaji wake” alisema Mhe. Rajabu Mzige ambaye ni Diwani wa Kata ya Manundu na ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Mazingira.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.