Mkurugenzi wa Mji wa Korogwe apokea Cheti cha Shukrani kutoka Shirika la US Peace Corps Tanzania
Kwaniaba ya Mkurugenzi wa Shirika la US Peace Corps Tanzania Bi. Stephanie de Goes, Afisa kutoka Shirika la US Peace Corps Tanzania Bw. Joel Onditi amemkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Bw. Tito Mganwa Cheti cha Shukrani baada ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe kuwapokea na kuishi nao vizuri Wataalamu (Volunteers) wa Nyanja mbalimbali kutoka Nchini Marekani. Cheti hicho cha Shukrani kilitolewa Julai 12, Mwaka huu katika Ofisi za Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Februari, Mwaka huu (2023) Wataalamu (Volunteers) Takribani Kumi na Sita wa Nyanja mbalimbali kutoka Nchini Marekani chini ya Shirika la US Peace Corps Tanzania, waliwasili katika Chuo cha Ualimu Korogwe (Korogwe TTC) kwa lengo la kujifunza Lugha ya Kiswahili na Utamaduni wa Kitanzania kwa ujumla kwa Wiki Kumi kabla ya kupelekwa katika vituo vya kazi hapa Nchini.
“Kwaniaba ya Mkurugenzi wa Shirika la US Peace Corps Tanzania Bi. Stephanie de Goes, natoa shukrani kwa Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Wananchi kwa ujumla kwa kuwapokea na kuishi nao vizuri Wataalamu kutoka Nchini Marekani” alisema Bw. Joel Onditi ambaye ni Afisa kutoka Shirika la US Peace Corps Tanzania wakati akikabidhi Cheti cha Shukrani. Bw. Joel alifafanua kuwa Shirika la US Peace Corps Tanzania litaendelea kuimarisha ushirikiano mwema baina ya Mji wa Korogwe na Shirika hilo katika kipindi chote cha Mafunzo.
“Kwaniaba ya Uongozi wa Halmashauri na Wananchi kwa jumla nitoe shukrani kwa Shirika la US Peace Corps Tanzania kwa kutukabidhi Cheti cha Shukrani kwa kuwapokea na kuishi nao vizuri Wataalamu kutoka Nchini Marekani” alisema Bw. Tito Mganwa ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Bw. Tito alifafanua kuwa Uongozi wa Mji wa Korogwe na Wananchi kwa ujumla ni wakarimu, wanawakaribisha Wataalamu wengine kutoka Shirika la US Peace Corps Tanzania kuja kujifunza mambo mbalimbali katika Mji wa Korogwe.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.