Mkurugenzi wa Mji wa Korogwe atembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha afya
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Ndugu Nicodemus Bei akiambatana pamoja na Mchumi wa Halmashauri hiyo Bi. Bernadetha January ametembelea mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi uliopo Kata ya Mgombezi. Lengo la kutembelea mradi huo wa Kituo cha Afya ni kukagua maendeleo ya ujenzi na kujionea hatua ulipofikia. Ziara ya kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya imefanyika Novemba 04, mwaka huu.
“Kituo hiki kitakapokamilika kitawasaidia Wananchi wa Mgombezi na maeneo ya jirani kupata huduma za afya karibu na maeneo yao” alisema Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wakati wa ukaguzi wa mradi huo. Ndugu Bei alifafanua kuwa Wananchi wote wanaishi maeneo ya pembeni ya Mji wa Korogwe ikiwapo Kata ya Mgombezi Halmashauri imeweka mkakati wa kuwapatia huduma za afya jirani na maeneo yao ili kuwapunguzia mwendo wa kwenda Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga).
“Halmashauri ya Mji wa Korogwe tunatoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi” alisema Bi. Bernadetha January ambaye ni Mchumi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Bi. Bernadetha alifafanua kuwa Serikali inatekeleza ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi kwa gharama ya Shilingi Milioni Mia Tano na tayari Serikali imeshatoa Shilingi Milioni Mia Mbili na Hamsini za awali kwa utekelezaji wa mradi huo.
Kwa upande mwengine, Ndugu Charles Kamugisha ambaye ni Mhandisi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alifafanua kuwa Mradi wa Kituo cha Afya cha Mgombezi utakuwa na majengo mawili, jengo la kwanza litakuwa la Mama, Baba na Mtoto na jengo la pili litakuwa la upasuaji. Kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Ndugu Kamugisha alifafanua kuwa mradi unatakelezwa kwa muda wa miezi Minne na ujenzi ulianza rasmi Oktoba mwaka huu na utakamilika Januari 2022.
Nae Ndugu Steven Mwita ambaye ni Mwananchi wa Kata ya Mgombezi alitoa shukrani kwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Serikali kwa ujumla kwa kuwapatia mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya kitakachosaidia kuwapatia huduma karibu na maeneo yao.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.