Shule ya Sekondari Semkiwa yapata Msaada wa Kompyuta
Shule ya Sekondari Semkiwa iliyopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe imepata msaada wa Kompyuta Ishirini na Tano (25). Msaada huo wa Kompyuta umetolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa ufadhili wa Taasisi ya Camara Education Tanzania. Msaada huo wa Kompyuta ulitolewa Agosti 23, Mwaka huu katika viwanja vya shule hiyo, huku Mgeni rasmi katika makabidhiano akiwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Jokate Mwegelo.
Msaada wa Kompyuta hizo Ishirini na Tano (25) ni sehemu ya Kompyuta Mia Moja (100) zilizotolewa na Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa ufadhili wa Taasisi ya Camara Education Tanzania zikiwa na Thamani ya Shilingi Milioni Thelasini na Saba. lengo la kutoa Msaada huo ni kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa na ujuzi katika Tehama utakaowasaidia maishani. Wilaya nyengine zilizonufaika na Msaada huo ni Handeni, Kibaha pamoja na Mji wa Kibaha.
“Nitoe shukrani kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania pamoja na Taasisi ya Camara Education Tanzania kwa kutupatia msaada wa Kompyuta katika Shule yetu” alisema Mhe. Jokate Mwegelo ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe na ndiye aliyekuwa Mgeni rasmi katika Makabidhiano ya Kompyuta hizo. Mhe. Jokate alifafanua kuwa Msaada wa Kompyuta hizo utawasaidi Wanafunzi kuongeza hamasa katika kujifunza Tehama Shuleni pamoja na kupata ujuzi.
Nae Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Bw. Tito Mganwa alitoa shukrani kwa Mamlaka ya Elimu Tanzania pamoja na Taasisi ya Camara Education Tanzania kwa kutoa Msaada wa Kompyuta katika Shule ya Sekondari Semkiwa huku akiwakaribisha kwa mara nyingine kuona ni namna gani wanaweza kusaidia kuongeza nguvu katika ujenzi wa Miundombinu pamoja na Vifaa mbalimbali katika maeneo mengine ya Mji wa Korogwe.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.