Viongozi ngazi ya Taifa, Mkoa watembelea vituo vya kutolea Chanjo ya Uviko -19
Viongozi wa Uhamasishaji wa Chanjo ya Uviko -19 kutoka Ngazi ya Taifa pamoja na Mkoa wa Tanga wametembelea Vituo mbalimbali vya kutolea Chanjo ya Uviko -19 vilivyopo katika Mji wa Korogwe. Lengo kuu la kutembelea Vituo hivyo ni kuongeza nguvu katika uelimishaji na uhamasishaji ili Wananchi wajitokeze kwa wingi katika kupata Chanjo ya Uviko -19. Ziara hiyo ya kutembelea Vituo vya kutolea Chanjo imefanyika Oktoba 02, mwaka huu ikiwa ni muendelezo wa Kampeni ya Utoaji wa Chanjo ya Uviko -19 Nyumba kwa Nyumba.
“Chanjo ya Uviko -19 ni hiari, lakini nawaomba tumieni fursa hii kupata chanjo ili kuimarisha kinga za mili yenu” alisema Dkt. Antoni Keya ambaye ni Mhamasishaji Ngazi ya Taifa wakati akizungumza na Wagojwa pamoja na Wataalamu wa afya wakati wa kutembeleaa Kituo cha Afya cha St. Raphael kilichopo Kijiji cha Kwamndolwa. Dkt. Keya alitoa nasaha kwa kusema kuwa Wananchi waache kusikiliza maneno ya mitaani na wasikilize ushauri kutoka kwa wataalamu wa Afya.
Katika hatua nyingine, Dkt. Keya alifafanua zaidi kuwa vita dhidi ya Ugojwa wa Uviko -19 sio jukumu la Serikali pekeyake. Jukumu hili ni la Wananchi wote wa Nchi hii hivyo itakuwa ni jambo la kizalendo Viongozi wa Dini, Wanasiasa, pamoja na Wahamasishaji wa maswala ya Kijamii wakaunga mkono jitihada za Serikali katika mapambano dhidi ya ugojwa huo.
“Achaneni na wapotoshaji wasiokuwa na nia njema katika Taifa hili (Tanzania), Chanjo ya Uviko -19 ni salama na haina shaka lolote” alisema Ndugu Jumanne Magoma ambaye ni Afisa Afya Mkuu Mkoa wa Tanga na Mhamasishaji wa Chanjo ya Uviko -19 Ngazi ya Mkoa wakati akizungumza na Vijana wanaojihusisha na Kilimo cha mpunga wakati wa kutembelea Kituo cha kutolea Chanjo ya Uviko -19 kilichopo Kijiji cha Mahenge.
Kwa upande mwengine, Ndugu Nasoro Sabuni ambaye ni Mwananchi wa Kijiji cha Mahenge alisema “changamoto kubwa inayosabibisha vijana kukataa kuchanja ni maneno ya mitandaoni, Serikali mmefanya jambo zuri kututembelea pamoja na kutuelimisha na sisi tutawaelimisha watu wengine”. Nae Dkt. Salma Sued, ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alitoa shukrani kwa Viongozi kutoka Ngazi ya Taifa na Mkoa kwa kutembelea Mji wa Korogwe kwa lengo la kuongeza nguvu katika uhamasishaji wa Chanjo ya Uviko -19.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.