Wananchi wa Mji wa Korogwe wahimizwa kujiunga na Elimu ya Watu Wazima
Wananchi wa Mji wa Korogwe walioshindwa kupata elimu katika utaratibu maalumu kutokana na changamoto mbalimbali wameshauriwa kujiunga na Elimu ya Watu Wazima ili kuepukana na changamoto ya kutojua Kuandika, Kusoma na Kuhesabu. Ushauri huo umetolewa na Diwani wa Kata ya Kwamsisi Mhe. Nassoro Mohamed aliyekua Mgeni rasmi wakati wa Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima katika Halmashuri ya Mji wa Korogwe. Maadhimisho hayo yalifanyika Oktoba 13, Mwaka huu katika Shule ya Msingi Manundu Mazoezi.
“Twendeni tukawahimize Wananchi waliokosa elimu katika utaratibu maalumu wajiunge na Elimu ya Watu Wazima ili kuepukana na changamoto ya kutojua Kuandika, Kusoma na Kuhesabu” alisema Mhe. Nassoro Mohamed ambaye ni Diwani wa Kata ya Kwamsisi wakati wa Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima. Mhe. Nassoro alisisitiza kuwa Wananchi watakaojiunga na Elimu ya Watu Wazima watanufaika na elimu katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ujuzi wa fani za kila aina kulingana na uhitaji wao.
“Halmashauri ya Mji wa Korogwe imejipanga vyema kuhakikisha inatoa Elimu ya Watu Wazima kwa kila kundi kulingana na uhitaji wao” alisema Bw. Aseri Mshana ambaye ni Afisa Elimu ya Watu Wazima katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Bw. Mshana alifafanua kuwa licha ya Halmashauri kujipanga vyema katika kuhakikisha inapunguza idadi ya watu wasiojua Kuandika, Kusoma na Kuhesabu lakini pia inampango wa kuhamasisha Wananchi kupata ujuzi wa fani mbalimbali kulingana na mazingira yao ili kujikwamua kimaisha.
Kwa upande mwengine, Wadau wa elimu, Viongozi mbalimbali pamoja na Wananchi walioshiriki katika Maadhimisho ya Juma la Elimu Ngazi ya Halmashauri Mwaka 2022, walitoa pongezi kwa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Serikali kwa ujumla kwa kuwaleta Wananchi wa Mji wa Korogwe katika Jukwaa Moja kwa lengo la kujadili changamoto za Elimu ya Watu Wazima na njia za kutatua changamoto hizo ili Wananchi waweze kwenda sambamba na maendeleo ya Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii wakiwa na elimu ya kutosha.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.