Dkt. Kimea: Madiwani wahimizeni Wananchi wakapate Chanjo
Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini Mhe. Dkt. Alfred Kimea amewashauri Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kuwahimiza Wananchi wajitokeze kwa wingi wapate chanjo ya Uviko -19 kwa lengo la kuimarisha kinga ya mwili ili iweze kupambana na ugonjwa wa Uviko -19. Kauli hiyo aliitoa Septemba 29, mwaka huu wakati wa kikao maalimu cha kujadili na kubadilishana mawazo juu ya utoaji wa Chanjo ya Uviko -19 katika Mji wa Korogwe.
“Waheshimiwa Madiwani namishauri muwahimize Wananchi wakapate Chanjo ya Uviko -19 alisema Mhe. Dkt. Alfred Kimea wakati wa kikao maalumu cha kujadili na kubadilishana mawazo juu ya utoaji wa Chanjo ya Uviko -19 kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe. Mhe. Dkt. Kimea alifafanua kuwa Chanjo ya Uviko -19 ni jambo la hiari lakini kutokana ni Kampeni ya Kitaifa na yenye manufaa ni vyema Madiwani wakaunga mkono jitihada za Mama (Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania).
Nae Mhe. Neema King’oso ambaye ni Kaimu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alitoa ushauri kwa Timu ya Kampeni ya Mpango Harakishi na Shirikishi wa Chanjo ya Uviko -19 kwa kusema “tumie muda mwingi katika kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuliko kuwalazimisha”. Mhe. King’oso alifafanua kuwa iwapo Mwananchi mmoja alielimishwa na kuhamasika vizuri, atasaidia kwenda kuwaelimisha Wananchi mwengine na kulifanya zoezi la kutoa Chanjo kuwa jepesi.
“Chanjo ya Uviko -19 ya Janssen Janssen ni salama na haina madhara yoyote kwa matumizi ya binadamu” alisema Dkt. Salma Sued wakati akitoa ufafanuzi kwa Madiawani kuhusu aina ya Chanjo itakayotolewa kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe. Dkt. Sued alifafanua kuwa katika Mji wa Korogwe kuna Vituo Kumi na Tatu (13) vya kutolea Chanjo. Na baada ya Kampeni ya utoaji wa Chanjo kumalizika, Vituo vilivyoteuliwa vitaendelea kutoa Chanjo kama kawaida.
Kuhusu idadi ya Chanjo zilizotolewa katika Mji wa Korogwe, Dkt. Sued alifafanua kuwa Mji wa Korogwe ulipatiwa Chanjo kiasi cha Elfu Mbili na Mia Moja (2100) na hadi kufikia Septemba 29, mwaka huu tayari Watu Elfu Moja na Tisini na Saba (1097) wameshapatiwa Chanjo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.