Halmashauri ya Mji wa Korogwe imeadhimisha siku ya wazee duniani, ambapo jamii hutambua na kuhamasisha, kulinda na kutetea haki za wazee duniani kote. Maadhimisho haya huadhimishwa Oktoba mosi ya kila mwaka, huku Kiwilaya yakiadhimishwa katika ukumbi wa mikutano katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Katika maadhimisho haya mgeni rasmi alikua Mh. Kissagwakisa Kasongwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe. Katika hotuba yake kwa wazee Mh. Kasongwa ametoa rai kwa watumishi wa umma kuwathamini na kuwasaidia wazee hasa kuwapatia huduma bora katika vituo vya afya. Ameongeza kuwa mtumishi yeyote ambaye atashindwa kuwahudumia wazee wanapohitaji huduma mbalimbali ni bora akatafuta kazi binafsi.
Maadhimisho haya huwa yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe unaogusa jamii katika kuwaenzi na kuwadhamini wazee. Kauli Mbiu ya mwaka huu inasema “Tuimarishe usawa kuelekea maisha ya uzeeni, uzee na kuzeeka hakuepukiki”. Katika maadhimisho haya pia mashirika binafsi yalishiriki katika kuungana na wazee duniani kote likiwemo shirika la Afriwag likingozwa na Bi. Magreth Ruhinda.
Katika risala iliyosomwa na Bwana Mtofi Hassan kwa mgeni rasmi kwa niaba ya wazee wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, wazee wameipongeza serikali kwa kuendelea kutambua changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo ikiwemo huhuma za afya kwa ujumla. Kwa upande mwingine Bi. Halima Saidi ambaye ameshiriki katika siku hii ya wazee duniani amesema kuwepo kwa siku hii ni kuonyesha kuwa wao kama wazee bado wanathaminiwa katika jamii.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.