Mji wa Korogwe kufanya kampeni ya chanjo ya Uviko-19 nyumba kwa nyumba
Halmashauri ya Mji wa Korogwe imeweka mikakati ya kufanya Kampeni ya Chanjo ya Uviko -19 Nyumba kwa Nyumba ili kuwarahisishia Wananchi kupata Chanjo ya Uviko -19 kwa haraka zaidi. Mkakati huo ulipangwa wakati wa kikao kazi cha wadau wa afya ulioshirikisha wataalamu kutoka Vituo vya Afya vya Serikali pamoja na Vituo binafsi. Kikao hicho kilifanyika Septemba 27, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga).
Kampeni ya Chanjo ya Uviko -19 katika Mji wa Korogwe itafanyika kwa Wiki Mbili, na tayari mchakato ulishaanza tokea Septemba 22, na itakwenda hadi Oktoba 05, mwaka huu. Katika Kampeni hii, Halmashauri ya Mji wa Korogwe inatarajia kutoa Chanjo ya Uviko -19 takribani Elfu Moja na Hamsini (1050), na Chanjo itakayotolewa kwa Wananchi ni aina ya Janssen & Janssen. Baada ya Kampeni kumalizika huduma ya Chanjo ya Uviko -19 itaendelea kutolewa kama kawaida katika vituo vyote vya kutolea Chanjo.
“Kampenini hii itahusisha Mji wote wa Korogwe, na itakua nyumba kwa nyumba mpaka tuhakikishe tumetimiza malengo tuliojiwekea” alisema Dkt. Salma Sued ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Dkt. Sued alifafanua kuwa chanjo ya Uviko -19 ni salama kwa matumizi ya binadamu na haina athari yoyote. Aliendelea kufafanua zaidi kwa kusema “Chanjo hii imethibitishwa Kimataifa na Kitaifa hivyo Wananchi wasiwe na hofu yoyote na wajitokeze kwa wingi katika vituo husika ili wapatiwe Chanjo”.
“Katika Kampeni hii ya Chanjo ya Uviko -19 tutahakikisha tunayafikia makundi yote ya watu popote yalipo” alisema Ndugu Seif Kibambe ambaye ni Mratibu wa Chanjo katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe wakati wa kikao kazi cha kuweka mikakati ya utoaji wa Chanjo katika Mji wa Korogwe.
Kwaupande mwengine, Ndugu Seif aliainisha Vituo vitakavyotumika kutoa Chanjo ya Uviko -19 ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga), Kituo cha Afya Majengo, St. Raphael, na St. Joseph. Pia kuna Zahanati ya Msambiazi, Mtonga, Mgombezi, Kilole, Kwamdulu, Kwakombo, Kwamsisi, Kwamndolwa pamoja na Zahanati ya Mahenge. Katika Vituo hivi huduma za Chanjo zitatolewa kuanzia Saa Mbili asubuhi hadi Saa Kumi na na Moja Jioni.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.