Mji wa Korogwe wajenga vyoo vya kisasa
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe akiambatana pamoja na Wakuu wa Idara ametembelea miradi wa ujenzi wa matundu ya vyoo vya kisasa kwa ajili ya shule mbalimbali za msingi. Ziara hiyo imefanyika Novemba 24, mwaka huu katika shule za Msingi zilizopo Mji wa Korogwe.
Halmashauri ya Mji wa Korogwe katika mwaka wa fedha 2020/2021 inatarajia kujenga matundu ya vyoo Hamsini na Tatu (53) katika shule mbalimbali za msingi kwa lengo la kupunguza changamoto za matundu ya vyoo zilizopo kwenye shule hizo. Ujenzi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani takribani Milioni Arobaini (40) pamoja na nguvu za wananchi.
“kwa kushirikiana na wananchi, Halmashauri tutahakikisha tunamaliza kabisa changamoto ya matundu ya vyoo katika shule za msingi” alisema Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe wakati wa ziara hiyo. Ndugu Bei alifafanua zaidi kwa kusema “miradi itakapokamilika itakuwa ni faraja kwa wanafunzi na kuwawezesha kusoma kwa furaha”
Nae Mhandisi Said Abuu ambaye ni Mhandisi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe na msimamizi wa miradi hiyo alifafanua kuwa Shule ambazo miradi tayari imekamilika ni pamoja na Shule ya Msingi Kilole matundu (8), Matondoro matundu (10), New Korogwe matundu (8), na Old Korogwe matundu (6).
Mhandisi Abuu aliendelea kufafanua kuwa shule ambazo ujenzi unaendelea ni pamoja na Shule ya Msingi Bagamoyo matundu (9), Kwamkole matundu (6) pamoja na Kwamngumi matundu (6). Kuhusu ukarabati wa matundu ya vyoo katika shule za msingi, Mhandisi Abuu alisema “ tayari tumeanza na Shule ya Msingi Mgombezi tukiifanyia ukarabati wa matundu ya vyoo kumi na nne (14)”.
Kwa upande mwingine, Ndugu Kassimu Kaoneka ambaye ni Afisa Elimu Msingi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe pamoja na Walimu Wakuu waliopata miradi hiyo wameishukuru Halmashauri kwa kutoa fedha pamoja wananchi kwa kuchangia nguvu kazi ili kufanikisha miradi hiyo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.