Mji wa Korogwe wazindua chanjo ya polio na surua
Halmashauri ya Mji wa Korogwe imezindua chanjo kwa ajili ya kukinga maradhi ya polio na surua, chanjo ambayo pia inatolewa kitaifa kwa nchi nzima kuanzia Oktoba 17 – 21 mwaka huu. Kwa Mji wa Korogwe uzinduzi huu umefanyika Oktoba 19,mwaka huu katika ofisi ya kata ya Old Korogwe.
Akizungumzia uzinduzi huo ndugu Aseri Mshana Afisa Elimu ya watu wazima aliyemuwakilisha Mkurugenzi alisema zoezi hili la utoaji chanjo linawahusu watoto wote kuanzia miezi tisa hadi miaka mitano hivyo ni muhimu watoto wenye umri husika kupata chanjo hii ili kujikinga na maradhi ya polio na surua. Ndugu Mshana alisisitiza kuwa mzazi au mlezi yoyote atakaebainika hajampeleka mtoto wake mwenye umri husika kupata chanjo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Nae Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Dr. Elizabeth Nyema alisema wamejipanga vyema na zoezi la chanjo na kuna vituo 13 vinavyotoaa chanjo katika mji mzima. Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 1:30 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni na chanjo itatolewa kwa siku tano mfululizo. Dr. Nyema alitoa angalizo kwa wanachi kuachana na mawazo potofu yanayotolewa na baadhi ya watu wasio na uzalendo na nchi hii na amewataka wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi katika vituo vya chanjo.
Kwa upande mwingine mratibu wa chanjo katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe Ndugu Seif Kibambe alisema wana vifaa na wataalamu wa kutosha kwa kila kituo na wamejipanga kuwapatia chanjo watoto 7385 wenye miezi tisa hadi miaka mitano. Nae Bi. Anna Omari ambaye ni mwananchi alisema amefurahi kuona serikali ilivyo na mikakati imara ya kutokomeza maradhi ya polio na surua hapa nchini kwani watoto ndio nguvu kazi ya baadae hivyo ni vyema kuwandalia misingi ya afya njema.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.