Mkuu wa Wilaya ya Korogwe akabidhi Mkopo wa Milioni 152 kwa Makundi Maalumu
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Basilla Mwanaukuzi amekabidhi Mkopo wa Shilingi Milioni 152 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu waliopo Mji wa Korogwe. Mkopo huo wa Shilingi Milioni 152 waliokabidhiwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu ulitolewa na Halmashauri ya Mji wa Korogwe ambao ni Asilimia Kumi zinazotokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri hiyo. Warsha ya kukabidhi mkopo huo imefanyika Machi 31, mwaka huu katika Kijiji cha Kwakombo kilichopo Mji wa Korogwe.
“Natoa wito kwa Maafisa Kilimo, Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Biashara waweze kutoa ushauri kwa wanufaika wa mikopo ili waweze kutumia mikopo hiyo kwa manufaa” alisema Mhe. Basilla Mwanukuzi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe wakati akukabidhi mkopo wa Shilingi Milioni 152 kwa Wanawake, Vijana na Watu Wenye ulemavu. Mhe. Mwanukuzi alisisitiza kuwa ni jambo la busara watu wote walionufaika na mkopo huo waweze kurejesha mkopo kwa wakati ili Vikundi vyengine viweze kunufaikia na mkopo huo.
“Halmashauri ya Mji wa Korogwe itaendelea kutoa mkopo wa Asilimia Kumi kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kadri fedha zinapopatikana” alisema Bi. Bernadetha January ambaye ni Mchumi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe aliyemuwakilisha Mkurugenzi. Bi. Bernadetha alifafanua kuwa utoaji wa mikopo wa Makundi Maalumu sio takwa la kiutashi bali ni agizo la kisheria, hivyo Halmashauri itaendeleo na jitihata za kutoa mkopo kwa Makundi Maalumu kwa lengo la kuhakikisha Makundi hayo nayajiimarisha kiuchumi.
Kwa upande mwengine, Bi. Chariy Sichona ambaye ni Afisa Maandeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alifafanua kuwa mkopo wa Shilingi Milioni 152 uliotolewa na Halmashauri umenufaisha Vikundi Ishirini na Sita. Katika Vikundi hivyo Wanawake wamepatiwa Shilingi Milioni 72,500,000, Vijana Shilingi Milioni 49,500,000 na Watu wenye ulemavu Shilingi Milioni 30,000,000. Bi. Charity alifafanua kuwa mkopo huo wa Shilingi Milioni 152 ulijumuisha utoaji wa Fedha taslimu, Bajaji, Mashine mbalimbali pamoja na Pikikipi.
“Kwa niaba ya Vikundi vyote natoa shukrani kwa Halmashauri ya Mji wa Korongwe na Serikali kwa ujumla ya Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kututhamini watu wa Makundi Maalumu na kutupatia mkopo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi” alisema Mzee Athumani Selemani ambaye ni Mlemavu wa miguu na mnufaika wa mkopo wa Bajaji wakati akitoa shukrani kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kwa niaba ya Vikundi vyote ambavyo ni wanufaika wa mkopo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.