Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe atembelea vyanzo vya mapato
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe Mhe. Francis Komba akiambatana pamoja na Kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo ametembelea vyanzo vya mapato vya Halmashauri kwa lengo la kuangalia mafanikio pamoja na changamoto zinazojitokeza wakati wa ukusanyaji mapato. Hatua hiyo ya kutembelea vyanzo vya mapato katika ni moja ya utekelezaji wa mkakati ya kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri. Ziara hiyo ya kukagua vyanzo mbalimbali vya mapato katika Mji wa Korogwe imefanyika Novemba 26, mwaka huu.
Katika ziara hiyo ya kutembelea vyanzo vya mapato, Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na Kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo walitembelea vyanzo mbalimbali vya mapato. Vyanzo hivyo vya mapato ni pamoja na Machinjio ya ng’ombe na mbuzi, Stendi ya John Kijazi, Soko la Kilole pamoja na Geti la ushuru wa mazao ya kilimo. Vyanzo vingine ni Soko la Old Korogwe, Stendi ya zamani, pamoja na Maeneo ya wazi.
“Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri tushirikiane kwa pamoja katika kuongeza mapato ya Halmashauri” alisema Mhe. Francis Komba ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na Diwani wa Kata ya Mtonga. Mhe. Komba alifafanua kuwa ili Halmashauri iweze kusonga mbele kimaendeleo inahitajka kuwa na mapato ya kutosha, hivyo ni muda muafaka Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri kuimarisha vyanzo vilivyopo pamoja na kubuni vyanzo vipya ili kuongeza mapato ya Halmashauri.
Katika hatua nyengine, Mhe. Francis Komba alisisitiza kuwa mtu yeyote atakayejaribu kuvujisha mapato ya Halmashauri bila kujali yeye ni nani, sheria itachukua mkondo wake ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani. Hata hivyo Mhe. Komba alitoa wito kwa Madiwani pamoja na Wataalamu wa Halmashauri kuwaelimishe Wananchi juu ya umuhimu wa Kolipa kodi katika vitega uchumi vya Halmashauri au kulipa ushuru katika maeneo mbalimbali. Iwapo Wananchi wataelimishwa vyema watalipa kodi au ushuru bila ya changamoto yoyote.
“Mheshimiwa Mwenyekiti ushauri wote uliotoa tumeupokea, sisi kama Wataalamu wa Halmashauri tumejipanga vyema kuhakikisha tunaongeza mapato katika Halmashauri yetu” alisema Ndugu Gaspa Mtui ambaye ni Kaimu Mueka Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Ndugu Mtui alifafanua kuwa katika jitihada za kuongeza vyanzo vipya vya mapato, Halmashauri tayari imeshaanzisha Kiwanda cha kufyatulia tofali za saruji. Kiwanda hicho kinauwezo wa kufyatua tofali Elfu Nne kwa siku moja.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.