Serikali yafungua maduka ya dawa katika Mji wa Korogwe
Halmashauri ya Mji wa Korogwe imefungua maduka mawili ya dawa za binadamu kwa lengo la kutoa huduma za dawa zilizo na bei nafuu kwa wagonjwa waliopo hospitalini pamoja na wananchi wote kwa ujumla. Maduka hayo mawili yameanza kutoa huduma kuanzia mwezi Juni mwaka huu ambapo duka moja lipo katika Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga) na duka jingine lipo katika Kituo cha afya cha Majengo.
Akizungumzia huduma za dawa zinazotolewa katika maduka hayo Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “kufunguliwa kwa maduka haya ya dawa ni muendelezo wa mikakati ya Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa wananchi”. Ndugu Bei aliendelea kufafanua kuwa huduma za dawa zinazotolewa katika maduka ya Serikali zitakuwa bora na dawa zitauzwa kwa bei nafuu ukilinganisha na maduka mengine.
Nae Dr. Elizabeth Nyema ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “ maduka ya dawa ya serikali tuliyoyafungua katika Mji wa Korogwe yatasaidia kuwapatia wananchi huduma zenye uhakika na vilevile kuongeza mapato katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe”. Kuhusu upatikanaji wa dawa kupitia Bima za afya, Dr. Nyema akifafanua kuwa maduka yote mawili yana mkakati wa kutoa dawa kwa kutumia Bima za afya za aina mbalimbali ingawa kwa sasa wameanza kutoa dawa kwa kutumia Bima ya Afya ya NHIF.
Kwa upande mwingine Dr. Herri ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga) na Dr. Samike ambaye ni Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Majengo walifafanua kuwa Maduka yote mawili ya dawa yatatoa dawa za magonjwa mbalimbali na huduma zitatolewa saa ishirini na nne (24) katika siku saba za wiki. Nae Bi. Halima Juma ambaye ni mteja aliyekuja kupata huduma za dawa katika duka la Majengo alisema “naipongeza Serikali kwa kufungua maduka ya dawa yanayotoa huduma kwa bei nafuu ukilinganisha na maduka mengine”.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.