Mradi wa ujenzi wa barabara Hoza-Ramia yenye urefu wa mita 690, unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu kwani mradi uko katika hatua za mwisho za uwekaji wa lami.
Kaimu Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Ndugu Dionis Ernest amesema “mradi huu umeanza tarehe 2/8/2018 ambao msimamizi wake ni NIMETA CONSULT LTD ambapo fedha za mradi huo zimetolewa na Benki ya Dunia chini ya mradi wa ULGSP”.
Ameongeza kuwa mpaka kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo kutagharimu jumla ya Tsh 843,063,358.00 pamoja na VAT ambapo barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami ngumu ambayo itakuwa na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito mkubwa, huku kazi ya kuweka lami ikitarajiwa kuanza siku chache kuanzia sasa.
Pia amesema shughuli inayoendelea kwa sasa ni kumalizia ujenzi wa barabara pamoja na ujenzi wa mifereji ili kuwezesha maji kupita kwa urahisi na pia kutakuwa na ufungaji wa taa za barabarani zitakazowezesha watumiaji wa barabara ya Hoza-Ramia kuona wanapokuwa wakitumia barabara hiyo.
Mkaguzi wa vifaa vya ujenzi wa NIMETA CONSULT LTD Bw. Lazaro Mveyange amesema “barabara imekamilika kwa 92% na kwa upande wa mifereji pia imekamilika kwa 97% kilichobaki ni kujengea vizuri kipande kidogo kilichobaki ili kuruhusu maji kupita vizuri”.
Aidha Bw. Mveyange amesema kuwa changamoto wanayokumbana nayo ni uelewa wa watumiaji wa barabara kwani hawafati alama zilizowekwa za kuzuia watu kupita au vyombo vya usafiri kwenye eneo la mradi hivyo kusababisha kuharibu sehemu ambazo ziko katika ujenzi.
Mfanyabiashara na mkazi wa eneo hili ambapo kuna ujenzi wa barabara Bw. Suleiman Ramadhan Msofe amesema “nashukuru kuona barabara hii inajengwa kwa kiwango cha lami na sisi wakazi wa hapa tutakuwa tunaenda sokoni huku tukitembea kwenye lami tofauti na mwanzoni”.
Bw. Msofe amesema “mtaa utafunguka kibiashara kwani tumesikia kutakuwa na ufungaji wa taa za barabarani ambazo zitatuwezesha kufanya shughuli za kibiashara mpaka usiku na huu ujenzi wa mifereji utasaidia maji kupita kwa urahisi hivyo hayatasumbua kama ilivyokuwa zamani ambapo maji yalikuwa yanakosa njia sahihi zakupita na kupelekea kuingia katika makazi ya watu, pia kutakuwa na usalama mkubwa kutokana na uwepo wa taa hizo watakazoweka kwenye barabara”
Ujenzi huu wa barabara ya Hoza-Ramia yenye urefu wa mita 690 utasaidia kufanya watumia vyombo vya usafiri na watumiaji wengine kufika kwa wakati sehemu mbalimbali wanazoenda bila tatizo lolote na pia kufungua fursa za biashara kwa wananchi wote wa Mji wa Korogwe na viunga vyake.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.