Mradi wa ujenzi wa madarasa mawili(2) na vyoo katika Shule ya Msingi Boma na Zung’nat zilizopo katika Halmashauri ya Mji Korogwe zimefikia katika hatua nzuri, ambapo madarasa na vyoo vipo katika hatua ya mwisho ya ukamilishwaji.
Mradi huo ambao umegharimu Tsh milioni 44 na laki 4 zikiwa ni za ujenzi wa Shule ya Misingi Boma, huku Tsh milioni 46 na laki 6 zikiwa ni kwaajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Zung’nat.
Fedha hizo ambazo zimetolewa na mpango wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) kupitia Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Magufuli katika jitihada za kupunguza uhaba wa madarasa na vyoo ili kuwafanya wanafunzi kusoma katika mazingira bora na salama.
Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Korogwe Bw. Kaoneka amesema kuwa mradi wa ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule zote mbili, Shule ya Msingi Boma na Zung’nat unaendelea vizuri na kwamba uko katika hatua za mwisho kukamilika.
Kwa upande wa Shule ya Msingi Boma kuna ujenzi wa madarasa mawili(2) na matundu manne ya vyoo(4), ambapo madarasa yote mawili(2) yako katika hatua ya uwekaji wa madirisha na kupiga plasta, huku vyoo vikiwa tayari na zoezi lililobaki ni uchimbaji wa mashimo ya vyoo.
Pia katika Shule ya Msingi Zung’nat kuna ujenzi wa madarasa mawili(2) pamoja na matundu sita(6) ya vyoo, ambapo kwa upande wa madarasa yako kwenye hatua ya kupiga plasta, vyoo vimeshajengwa na vimekamilika.
Aidha ushiriki wa jamii kwa baadhi ya maeneo katika ujenzi wa madarasa na vyoo ni mdogo haswa katika ujenzi wa Shule ya Msingi Boma kulinganisha na ujenzi wa shule ya msingi Zung’nat ambapo wananchi wameshiriki kikamilifu katika kusaidia ujenzi wa madarasa.
Jamii inashiriki katika ujenzi wa madarasa na vyoo kwa kuchota maji, kukusanya kokoto, kuchimba msingi na kubeba maji na hivyo kusaidia kupunguza gharama na kuharakisha ujenzi.
Changamoto kubwa katika ujenzi wa madarasa na vyoo ni pamoja na uhaba wa maji hasa ukizingatia kuwa hiki ni kipindi cha kiangazi.
Bw. Kaoneka amesema ‘bado kuna uhaba wa madarasa kama watatokea wadau wengine wanaweza kutusaidia kujenga madarasa mengine’.
Mradi wa ujenzi huu wa madarasa pamoja na vyoo katika Shule ya Msingi Boma na Zung’nat unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.