Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe -Magunga imeanza kupokea vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya Sh. milioni 100 kupitia Mfuko wa Mama, ulioanzishwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuimarisha huduma za afya na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopewa rufaa.
Akizungumza Januari 8, 2026 katika ziara ya Mbunge wa Korogwe Mjini Charles Njama, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Paul Anyabwile, amesema miongoni mwa vifaa vilivyopokelewa ni mashine ya dawa ya usingizi (Anesthesia Machine), ambayo itakapokamilika kufungwa na kuanza kutumika itaongeza uwezo wa hospitali kutoa huduma za upasuaji kwa ufanisi zaidi.
Anyabwile amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya, hali iliyoifanya Hospitali ya Magunga kunufaika na vifaa hivyo muhimu, huku akibainisha kuwa vifaa vingine vinaendelea kuwasili hospitalini hapo.
Aidha, amemshukuru Mbunge Njama, kwa kutembelea hospitali hiyo na kuahidi kuwa wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, wakimuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika dhamira ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya.
Naye Mbunge Njama ambaye aliambatana na Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ameipongeza timu ya wataalamu wa hospitali hiyo kwa kujituma kwao katika kutoa huduma kwa wananchi.
Pia, amepongeza ubunifu wa hospitali hiyo wa kujenga njia za watembea kwa miguu zitakazorahisisha kupeleka wagonjwa chumba cha upasuaji na wodini huku akichangia Sh.milioni moja kwa ajili ya kuendeleza ujenzi huo.
Hata hivyo, ametoa wito kwa wadau wengine kuchangia ujenzi wa njia hizo ili kuboredha zaidi mazingira ya utoaji huduma.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.