Baraza la madiwani lapitisha ujenzi wa kituo cha afya
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe limepitisha Ujenzi wa Kituo cha afya katika Kata ya Kwamsisi pamoja na ununuzi wa mashine mpya ya mionzi (x-ray) kwa ajili ya Hospitali ya Mji wa Korogwe. Baraza hilo ambalo ni la robo ya pili katika mwaka wa fedha 2019/ 2020 limefanyika Machi 12, mwaka huu katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Akizungumzia mchakato huo Mh. Hillary Ngonyani ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “ mpango wa ujenzi wa Kituo cha afya cha Kwamsisi ni moja ya mikakati ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe katika kuboresha sekta ya afya na tutaendelea na ujenzi wa vituo katika Kata vyingine”.
Nae Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Mji wa Korogwe alisema kuwa Baraza la Madiwani limepitisha ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Kwamasisi ili kuwapatia wananchi huduma za afya baada ya baadhi ya huduma kukosekana katika zahanati ya Kwamsisi hadi Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga) ambako ni mbali na eneo hilo.
Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Kwamsisi Mh. Nassoro Hassan alilishukuru Baraza la Madiwani kwa kupitisha mchakato wa ujenzi wa Kituo cha afya cha Kwamsisi na alisema “ ujenzi wa kituo hiki ni jambo la faraja kwa wananchi wa kata yangu, wananchi wataweza kupata huduma za afya za huhakika kwa ukaribu zaidi’’.
Katika hatua nyingine Madiwani walipitisha ununuzi wa mashine mpya ya mionzi (x-ray) ambayo itakuwa ni maalumu kwa ajili ya Hospitali ya Mji wa Korogwe (Magunga). Kupatikana kwa mashine mpya kutasaidia kupunguza changamoto za huduma ya mionzi baada ya mashine iliyopo kuharibika. Nae Dkt. Elizabeth Nyema ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema kuwa mashine hiyo mpya itanunuliwa kutoka Shirika la usambazaji dawa la Medical Store Depatment (MSD) kwa gharama za takribani milioni mia tatu tisini.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.