Kidato cha sita Korogwe Girls warudi shuleni
Wanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Korogwe Girls wamerudi shuleni baada ya kukaa nyumbani kwa muda wa takribani miezi miwili kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona (Covid – 19). Wanafunzi walianza kuwasili shuleni kuanzia Mei 30, na Shule ilifunguliwa rasmi June 1, mwaka huu baada ya agizo la Serikali kutaka wanafunzi wote wa vyuo wapamoja na kidato cha sita warudi shuleni kuendelea na masomo.
Akizungumzia ujio wa wanafunzi Bi. Annisia Mauka ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Korogwe Girls alisema “uongozi wa shule pamoja na watalaamu wa afya waliopo shuleni tumejiandaa vyema kuwapokea wanafunzi na mpaka sasa mambo yote yanakwenda vizuri”. Bi Mauka aliendelea kufafanua kuwa mpaka kufikia June 2, mwaka huu tayari wanafunzi 308 wameshawasili kati ya wanafunzi 362 waliosajiliwa.
Kwa upande wa masomo Bi Mauka alisema “tumejipanga vizuri kuwafundisha wanafunzi ili waweze kujiandaa vyema na mitihani ya kidato cha sita inayotarajiwa kuanza June 26, mwaka huu.” Pia Bi Mauka alifafanua kuwa tayari wameshatoa elimu ya kutosha kwa wanafunzi jinsi ya kujikinga na ugojwa wa Corona (Covid – 19) na vilevile kufuata maelekezo ya kiafya ambayo ni kuwapima joto wanafunzi wanapowasili shuleni, wanafunzi kuvaa barakoa, kukaa mita moja kutoka meza moja hadi nyingine pamoja na kuweka maji safi tiririka na sabuni katika maeneo mbalimbali ya shule.
Nae Dr. Joyceline Sombo ambaye ni Daktari katika Zahanati ya Shule ya Korogwe Girls alisema “wanafunzi wote 308 waliwasili wako vyema baada ya kuwapima joto la mwili na matokeo kuonesha wanajoto la wastani”. Dr. Sombo alifafanua kuwa wanafunzi wana furaha ya kutosha na hawana hofu yoyote na ugonjwa wa Corona (Covid -19), hofu kubwa ya wanafunzi iko kwenye mitihani ya kumalizia masomo yao. Kwa upande wa wanafunzi walitoa shukurani kwa uongozi wa shule na Serikali kwa ujumla kwa maandalizi mazuri pamoja na kuweka mikakati imara ya masomo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.