Kituo cha afya cha Majengo chaanzisha kliniki ya magojwa ya macho
Kituo cha afya cha Majengo kilichopo katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe kimeanzisha kliniki ya magojwa ya macho. Huduma za uchunguzi pamoja na matibabu ya macho katika kliniki hiyo imeanza kutolewa kunzia Februari 6, mwaka huu.
Akizungumzia kliniki hiyo, Ndugu Lucas Zimamoto ambaye ni Afisa muuguzi msaidizi anayehusika na matibabu ya macho alisema “kituo cha afya Majengo kimeanzisha kliniki ya magonjwa ya macho lengo kuu ni kuwasogezea wananchi huduma karibu baada ya huduma hii kupatikana sehemu moja ambapo ni Hospitali ya Mji wa Korogwe “.
Ndugu Zimamoto aliendelea kufafanua kuwa huduma zinazotolewa katika kliniki hiyo ni uchunguzi wa magojwa ya macho, utoaji wa dawa za macho, na upimaji wa miwani za macho. Huduma nyingine ni upasuaji wa mtoto wa jicho pamoja na utoaji wa uhauri kuhusu maswala mbalimbali ya macho.
Tokea kuanzishwa kwa kliniki hiyo, wagojwa takribani ishirini na saba (27) wameshapatiwa huduma mbalimbali za macho. Licha ya mafanikio yaliyopatikana kwa muda mchache, kliniki pia inampango wa kushirikiana na taasisi nyingine zinazojishughulisha na matibabu ya macho ili kufanya uchunguzi wa kina kwa wagonjwa pamoja na upasuaji wa mtoto wa jicho. Taasisi hizo ni pamoja na KCMC, Medwell, CBM na Sight Servers.
Kwa upande mwingine Bi. Jamila Khatibu ambaye anasumbuliwa na matatizo ya macho alisema kuwa anaishukuru kliniki ya macho iliyopo kituo cha afya Majengo kwani tokea apate huduma katika kliniki hii macho yake yameimarika vyema. Kuhusu siku za huduma, kliniki hutoa huduma kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa. Huku kliniki ikifunguliwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi alasiri.
Nae Dkt. Elizabeth Nyema ambaye ni Mganga mkuu katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “kufunguliwa kwa kliniki hii ya magojwa ya macho katika kituo cha afya Majengo ni mkakati wa kufikia malengo ya sera ya afya inayotaka kila kituo cha afya kutoa huduma za matibabu ya macho pamoja na kinywa “. Dkt. Nyema aliendelea kusisitiza kuwa kliniki imejipanga vizuri kuwapatia wananchi huduma bora ya macho.
Katika hatua nyingine, Bwana Gino Mbwilo ambaye ni Katibu wa afya katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe alitoa ushauri kwa kusema “wananchi ni vizuri kuwahi hospitali pindi wanapopata dalili za magonjwa ya macho kabla ya tatizo kuwa kubwa “.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.