Madiwani wa Mji wa Korogwe wakutana katika kikao maalumu, Wajadili namna ya kupokea maeneo ya utawala kutoka Wilaya ya Korogwe
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Korogwe limekutana katika kikao maalumu ambacho kimejadili namna ya kujiandaa na mapokezi ya baadhi ya maeneo ya utawala kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe. Kikao hicho kimefanyika Januari 7, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano uliopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Akiwasilisha taarifa hiyo kwa Waheshimiwa Madiwani, ndugu Charles Mtali ambaye ni Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe akimuakilisha Mkurugenzi alisema kuwa maeneo yanayopendekezwa ni Kata zote zilizopo Tarafa ya Korogwe na Magoma ambazo ziko kumi (10), Vijiji arobaini na moja (41) pamoja na Vitongoji miambili na tano (205).
Ndugu Mtali Aliendelea kufafanua kuwa mchakato huu umetokana na kuhama kwa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe kwenda eneo la Kwasunga katika kutekeleza agizo la Mh. Dkt. John Pombe Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na agizo la Mh. Selemani Jafo Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Nae Mh. Hillary Ngonyani ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe baada ya kupokea taarifa hizo alisema kuwa maeneo watakayopokea yatakua karibu na makao makuu ya Halmashauri ya Mji wa Korogwe hivyo wananchi watapata huduma za jamii kwa wepesi. Kwa upande mwingine Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe walisema kuwa wako tayari kupokea maeneo hayo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.