Mji wa Korogwe waadhimisha Siku ya Wazee Duniani
Halmashauri ya Mji wa Korogwe imeungana na ulimwengu wote kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani. Siku ambayo huadhimishwa ifikapo Oktoba 1, ya kila mwaka. Katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuwatambua Wazee na kutambua changamoto walizonazo pamoja na kutafuta njia sahihi ya kutatua changamoto zao. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “familia na jamii tuwajibike kuwatunza wazee”.
Akizungumzia Siku ya Wazee Duniani Mh. Kissa Kasongwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe na ndiye mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alisema “mdau wa kwanza wa kumtunza mzee ni familia yenyewe”. Mh. Kasongwa alitoa nasaha kwa Vijana kwa kusema “vijana ni vyema kuhakikisha wazee walioko kwenye familia zetu tunawatunza ipasavyo”.
Kwa upande wa Ndugu Frank Fuko ambaye ni Afisa Ardhi na Mipango Miji katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe anayemuwakilisha Mkurugenzi alisema “tutahakikisha wazee wote wanapata huduma bora na kwaharaka zaidi watakapofika katika idara mbalimbali za Serikali”.
Nae Bi Felista Mkagulu ambaye ni Mwenyekiti wa Mabaraza ya Wazee katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema”. naiomba Serikali kutoa kipaumbele kwa wazee wakati wa kupata huduma katika ofisi za serikali” Kwa upande mwengine, Wazee walioshiriki katika maadhimisho hayo waliishukuru Serikali na wadau wote kwa kufanikisha maadhimisho ya mwaka huu.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.