Mji wa Korogwe wapitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021
Baraza la Madiwani katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe limepitisha bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021. Bajeti ambayo ndiyo taswira ya kimaendeleo katika makusanyo na matumizi ya Halmashauri. Baraza lilipitisha bajeti hiyo Januari 31, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano uliopo Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021, Halmashauri ya Mji wa Korogwe inakisia kukusanya na kutumia shilingi bilioni 26.06 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato. Bajeti hii imeongezeka kutoka shilingi bilioni 19.8 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 hadi kufikia shilingi bilioni 26.06 kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ongezeko hili ni sawa shilingi bilioni 6.2.
Bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021 imetoa vipaumbele katika mambo yafuatayo: Kuongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwa kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha timu ya ufuatiliaji na ununuzi wa mashine za risiti (POS), Kutenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa matunzo ya miradi iliyopo katika Halmashauri kama vile soko jipya la Kilole pamoja na Kituo kikuu cha mabasi kilichopio Kilole.
Vipaumbele vingine ni pamoja na kutenga asilimia kumi (10) ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Kusimamia upatikanaji wa maslahi na motisha kwa watumishi, na maslahi ya viongozi kwa maendeleo ya ustawi wao. Kutenga fedha asilimia arobaini (40) kwa ajili ya kuchangia miradi ya maendeleo, pamoja na Kukamilisha miradi iliyobakia na kuendeleza miradi mipya ya maendeleo kwa njia kushirikisha nguvu kazi za wananchi (msaragambo).
Kwa upande mwingine Bi. Bernadetha January ambaye ni Mchumi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe alifafanua kuwa mpango huu wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/2021 unalenga kushirikisha wananchi katika kukuza uchumi na kupunguza umasikini. Bi. January aliendelea kusisitiza kuwa mpango wa bajeti hiyo umeandaliwa kwa kushirikisha wananchi kuanzia ngazi za Kata, Mtaa hadi Vijiji.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.