Mkuu wa Wilaya ya Korogwe asisitiza uwekezaji katika mkonge
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa ameitaka Halmashauri ya Mji wa Korogwe kukamilisha kwa haraka kitalu cha mkonge chenye ukubwa wa Hekari Kumi ikiwa ni mkakati wa Serikali kwa kila Halmashauri Mkoani Tanga kuandaa eneo la Hekari kumi kwa ajili ya kitalu cha mkonge. Mhe. Kasongwa Alitoa agizo hilo wakati wa Baraza la Madiwani lililofanyika Aprili 30, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
“Wataalamu wa kilimo tekelezeni agizo la kilimo cha mkonge kwa asilimia mia moja” Alisema Mhe. Kissa Gwakisa Kasongwa wakati akitoa ushauri kwa wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe katika kuwekeza kwenye kilimo cha mkongwe. Nae Mhe. Francis Komba ambaye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe na ni Diwani wa Kata ya Mtonga alisema “agizo la Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kuhusu kilimo cha mkonge tumelipokea na tutalifanyia kazi kwa asilimia Mia Moja”.
Nae Ndugu Nicodemus Bei ambaye ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe alisema “tayari tumeiandikia barua Bodi ya Mkonge Tanzania kuomba eneo lenye ukubwa wa Hekari Mia Mbili kwa ajili ya kilimo cha mkonge”. Ndugu Bei alifafanua zaidi kuwa mchakato wa kitalu cha cha mkonge chenye ukubwa wa Hekari Kumi umeshaanza na kitalu kipo jirani na Shule ya Msingi Kwamsisi katika Kata ya Kwamsisi.
Kwaupande mwengine, Ndugu Abdul Nguzo ambaye ni Katibu wa Wazazi Jumuia ya Chama cha Mapinduzi Korogwe Mjini alisema “ uongozi wa Chama Cha Mapinduzi katika Mji wa Korogwe tayari tumeshaanza kuhamasisha wananchi kuwekeza kwenye kilimo cha mkonge ili kujiongezea kipato na kuondokana na umaskini”.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.