Mkuu wa Wilaya ya Korogwe atembelea miradi ya maendeleo
Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhe. Basilla Mwanukuzi akiwa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Korogwe pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe ametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Lengo la kutembelea miradi hiyo ni kuangalia jinsi Taasisi za Serikali zinavyotekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi katika kuwaletea Wananchi maendeleo. Ziara hiyo ya kutembelea miradi imefanyika Julai 23, mwaka huu katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Korogwe.
“Naomba tuendeleze ushirikiano wetu baina ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Halmashauri katika usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo” alisema Mhe. Basilla Mwanukuzi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Korogwe wakati alipotembelea miradi ya maendeleo. Mhe. Mwanukuzi alifafanua kuwa Wahusika wanazopewa usimamizi wa miradi wanatakiwa kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili miradi iweze kuwaletea Wananchi maendeleo.
“Natoa pongezi kwa Mkurugenzi pamoja na Wataalamu wote wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo” alisema Mhe. Dr. Alfred Kimea ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini wakati alipotembelea miradi ya maendeleo. Mhe. Dr. Kimea alisisitiza kuwa yeye pamoja na Ofisi yake wataendelea kushirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe pamoja na Taasisi nyingine za Serikali zilizopo Mji wa Korogwe katika kuwalete Wananchi maendeleo.
Kwa upande mwengine, Bi. Bernadetha January ambaye ni Afisa Mipango katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe anayemuwakilisha Mkurugenzi alisema “ Halmashauri ya Mji wa Korogwe itaendelea kusimamia ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa Wananchi wa Mji wa Korogwe”. Katika hatua nyingine Bi. Bernadetha alitoa shukrani kwa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Korogwe kwa kutembelea miradi ya maendeleo na kujionea jinsi ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyotekelezwa kwa vitendo.
Katika ziara hiyo Miradi iliyotembelewa na Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Korogwe ilijumuisha Kikundi cha Walemavu cha Tumaini Jema kilichopo Mtonga Juu, Ujenzi wa Madarasa katika Shule ya Msingi Kwamngumi, Ujenzi wa Maabara katika Shule ya Sekondari Joel Bendera pamoja na kuangalia jinsi Shule ya Sekondari Kimweri inavyonufaika na mradi wa umeme unaotekelezwa na Tanesco. Miradi mingine iliyotembelewa ni Barabara ya Kibo Mamanka iliyopo katika eneo la Kwamkole unaotekelezwa na Tarura, Mradi wa umeme unaotekelezwa na Tanesco uliopo katika eneo la Makwei, na Mradi wa Ujenzi wa Tanki kubwa la Maji unaotekelezwa na Ruwasa uliopo eneo la Rwengela Relini.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.