Ujenzi wa kituo cha afya Majengo umekamilika kwa asilimia 90 tangu ujenzi ulipoanza mwaka jana, na hivyo asilimia 10 tu za ujenzi huu zinatarajiwa kukamilika ifikapofika mwezi wa nne mwaka huu.
Kaimu mganga mkuu wa kituo cha afya Majengo Bw. Salim Bori amesema ‘ ukarabati na utanuzi wa kituo hiki umekamilika kwa asilimia 90 ambapo asilimia 10 zilizobaki ni za uwekaji wa umeme na maji tu” aliongeza kuwa miundombinu yote ya umeme na maji iko tayari kilichobaki ni upitishaji wa umeme huo pamoja na maji.
Salim Bori amesema kuwa majengo yote matano ambayo ni wodi ya wazazi, jengo la X-ray (Mionzi), jengo la upasuaji, jengo la maabara pamoja na nyumba ya mtumishi yamekamilika na hivyo yanaweza kutumika muda wowote kuanzia sasa mara baada ya kukamilisha uwekaji wa umeme na maji.
Pia amesema kuwa changamoto ilikuwa ufinyu wa eneo lakini mara baada ya kukamilika kwa majengo hayo kila kitu kitakuwa sawa na watu watapata huduma kwa urahisi tofauti na ambavyo ilivyo kwa sasa.
Aidha mhasibu wa kituo cha afya Majengo Bakari Kawambwa amesema shilingi milioni 500 ambazo walizipata mwaka jana mwezi wa tano kutoka serikalini, zimetumika vizuri na kusababisha majengo yote matano kukamilika kwa wakati bila kusuasua.
Ameongeza kuwa matarajio yao baada ya kukamilika kwa ujenzi huu, watu laki moja wataweza kuhudumiwa na hivyo huduma hii itawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi. Amesema madaktari na wataalamu wa mionzi na maabara wapo kwaajili ya kutoa huduma bora mara baada ya kituo hicho kukamilika.
Kwa upande wa wananchi wamekuwa na muitikio mkubwa tangu kuanza kwa mradi huu wa ujenzi wa kituo cha afya hadi kufikia hatua ya mwisho na kupongeza juhudi zinazofanywa na serikali ya awamu wa tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ili kupata huduma bora za afya.
Ujenzi wa vituo vya afya ni jambo linaloacha alama nzuri inayoonyesha utekelezaji wa kazi za serikali ili kutoa huduma bora kwa wananchi wao na kuwasogezea huduma za afya karibu na makazi yao.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.