Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ni magonjwa ambayo yamo ndani ya jamii hasa jamii masikini.Magojwa hayo ni Matende na Mabusha, Kichocho, Minyoo ya tumbo, Usubi, na Trakoma.
Mratibu wa mafunzo kutoka Wizara ya Afya Dk. Joyceline Sambo amesema dhumuni la mafunzo hayo ni kuwafanya viongozi wanaoongoza jamii kuwa na uelewa na pia kutoa elimu juu ya madhara ya magonjwa hayo kwani hayapewi kipaumbele kama yalivyo magonjwa mengine, mafunzo hayo yametolewa kwa viongozi mbalimbali wakiwemo madiwani.
Ameongeza kuwa kwakuwa wao ni viongozi hivyo kupitia wao wataweza kuwafikia wananchi wao kwa karibu zaidi.
Dk Sambo amesema “magonjwa haya ni kama kichocho ambacho husababishwa na minyoo ya jamii ya Schistosoma ambapo binadamu hueneza vimelea vya ugonjwa huu kwa kutojisaidia kwenye choo na kupelekea kinyesi/ mkojo kuchangamana na vyanzo vya maji, lakini pia kuna ugonjwa wa matende na mabusha ambao husababishwa na minyoo aina ya Wechereria Bancrofti unaosambazwa na mbu aina zote”.
Amesema ugonjwa wa usubi ambao husababishwa na minyoo, minyoo hiyo inaenezwa na inzi weusi wadogo ambao hukaa kandokando ya mito yenye maji yaendayo kasi, magonjwa mengine ni trakoma na minyoo ya tumbo.
Dk Sambo ameiomba jamii kutunza mazingira kwani magojnwa haya husababishwa na utunzaji mbovu wa mazingira na usafi kwa ujumla.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Mgombezi Bw. Omary Kassim Chafesi amesema “nimefurahia mafunzo haya na kuyapokea vizuri na kwa jinsi nilivyoelewa nitawaelimisha jamii ninayoiongoza katika mikutano yangu yote ya nje na ndani”.
Diwani Omary ameongeza kuwa magonjwa haya husumbua jamii za watu wenye hali ya chini na wao kupuuzia kwa kujua kuwa ni magonjwa ya kawaida lakini kutokana na uelewa alioupata kupitia mafunzo haya atahakikisha anatoa mafunzo kwa jamii ili waepukane na magonjwa.
Pia amesema kuwa atatoa elimu kwa jamii juu ya usafi wa miili yao na mazingira yanayowazunguka ili kusaidia kutunza vyanzo vya maji na kuepukana na magonjwa.
Nae diwani wa viti maalum Wilhelma Mpangala amesema “ semina nimeikubali na nimeipenda kutokana na elimu kubwa niliyoipata leo kwakuwa sikujua kwamba hata sisi wanawake tuna mabusha lakini kupitia elimu hii nimejua”.
Aidha ameongeza kuwa “nitahakikisha naelimisha jamii yangu yote na nitahakikisha nawaambia wale watakaotoa dawa kufatilia kwa makini kama watu wamekunywa kweli”.
Nchini Tanzania wananchi wote, wapo hatarini kuambukizwa magonjwa haya. Inakadiriwa kuwa watu milioni 5 wameshaathirika na mojawapo ya magonjwa hayo.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.