Wataalamu wa kilimo Wilaya ya Korogwe wakutana, waweka mikakati ya kilimo bora kuelekea uchumi wa viwanda
Wilaya ya Korogwe imekutanisha wataalamu mbalimbali wa kilimo pamoja na wakulima katika kuweka mikakati ya kilimo cha kisasa ili kufikia malengo ya uchumi wa viwanda hapa nchini. Wadau hawa wa kilimo walikutana Desemba 10, mwaka huu katika ukumbi wa mikutano uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe.
Mkutano huu ulifunguliwa na Dkt. Elizabeth Nyema ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Korogwe akimuwakilisha Mkurugenzi wa Mji. Lengo la mkutano huu ni kuwaleta pamoja wadau wote wa kilimo katika Wilaya ya Korogwe ili kujadiliana pamoja na kuweka mikakati ya kuimarisha kilimo cha kisasa kuelekea uchumi wa viwanda hapa nchini.
Katika mkutano huo Dkt Nyema alifafanua kuwa katika kufikia malengo ya uchumi wa viwanda hapa nchini ni muhimu wakulima kuzalisha mazao bora ambayo yatasaidia kutupatia chakula pamoja na malighafi katika kuzalisha bidhaa mbalimbali za viwandani. Aliendelea kufafanua kuwa ili tupate mazao bora ni muhimu kufuata kanuni za kilimo bora ikiwa ni pamoja na kuandaa mashamba kwa wakati, kuchagua mbegu bora, kupanda kwa wakati, kutumia mbolea na dawa za kuulia wadudu vilevile kuvuna mazao kwa wakati.
Nae Bwana Venance Ndunga ambaye ni wakala wa mbegu kutoka kampuni ya Seed – Co alisema “wakulima ni vyema kufahamu hali ya hewa ya eneo lao, hii itawasaidia kuchagua mbegu sahihi itakayowapatia mazao yenye tija”. Vilevile Ndugu Salehe Kombo ambaye ni mtaalamu wa kilimo kutoka taasisi ya TOSCI inayosimamia ubora wa mbegu za mazao ilitoa ushauri kwa wauzaji wa mbegu kuwa ni muhimu kuhifadhi mbegu vizuri ili ziendelee kubaki na ubora wake hadi mkulima atakapochukua kwa ajili ya kupanda.
Kwa upande mwingine mdau wa kilimo Bwana Abdallah Issa alisema kuwa amefarijika kupata elimu ya kilimo bora, elimu hii itamsaidia kuzalisha mazao yenye tija, vilevilea amepata mbinu za kutosha ili kukabiliana na wanyama waharibifu wa mazao.
Korogwe Tanga Tanzania
S.L.P: 615 Korogwe
Simu: 0272650050
Simu ya Kiganjani:
Barua Pepe: info@korogwetc.go.tz
Copyright©2018 Korogwe Town Council. All rights reserved.